KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

December 20, 2014

CHADEMA:UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA ULIHUJUMIWA


Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema imesema tathmini yao kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka huu imebaini kuwa ulihujumiwa.
Pia, kimewataka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia kujitathmini na kuchukua hatua za kuwajibika kwa kujiuzulu kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo uchaguzi huo.
Hayo yalisemwa jana jijini hapa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa (pichani)wakati akitoa maazimio ya kikao cha siku moja cha kamati hiyo kilichofanyika juzi kikiwa na ajenda moja ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Matatizo yaliyojitokeza yameanzia kwa Pinda na Ghasia, kwa kutoa kanuni na miongozo ambayo imefanya vyama vya upinzani hususan wagombea wa Ukawa kuenguliwa kwa mapingamizi yaliyokuwa na lengo la kuibeba CCM,”
“Katika maeneo ambayo upinzani ulishinda bado matokeo yalikuwa ngumu kutangazwa na wakati mwingine damu ilimwagika, hii yote ni mtawala kutaka kuendelea kung’ang’ania madaraka, hujuma za aina hii hatuwezi kuendelea kuzikubali kuendelea kutokea katika nchi inayojinasibu kuwa ya kidemokrasia,” alisema Dk Slaa.
Aliongeza: “Tunalaani vikali na kutoa onyo kali kwa watawala kushindwa kuheshimu demokrasia ambayo Watanzania wameamua kuitumia kupitia sanduku la kura kwa kuwapiga na kuwaua...licha ya hujuma hizo, lakini bado tumefanya vizuri na hasa katika majimbo ya CCM na wanayotoka mawaziri.”
Kuhusu maeneo ambayo uchaguzi umekuwa ukirudiwa baada ya kuahirishwa kutokana na matatizo kadhaa, Dk Slaa aliwaomba Watanzania kutumia fursa hiyo kufanya mabadiliko ya kiutawala.
“M4C (Vuguvugu la Mabadiliko) linaanza kufanya kazi, tunawashukuru Watanzania kwa kutuunga mkono hususan vyama vya Ukawa na waendelee katika kufanya hivyo maeneo ambayo uchaguzi unarudiwa ili kutoa funzo kwa CCM kwamba haina hati miliki ya nchi hii.”
“Viongozi wetu waliochaguliwa ikitokea wanatuhumiwa kwa vitendo vya rushwa kamwe chama hakitawavumilia viongozi hao na tutachukua hatua mara moja bila kusita ikiwamo za ndani ya chama na hata kuwashtaki mahakamani,” alisema.
Katika matokeo ambayo wameyapata ya uchaguzi huo alisema, wamefanikiwa kuongoza mamlaka za miji na miji midogo kutoka miwili ya Hai na Karatu hadi 30 pande zote za nchi.
Baadhi ya mamlaka hizo na majimbo katika mabano ni Namanyere (Nkasi),Bomang’ombe,Tunduma (Mbozi Magharibi), Katoro (Busanda), Chato (Chato), Mbalizi (Mbeya Vijijini), Sengerema (Sengerema), Bunda (Bunda), Tarime (Tarime), Kahama (Kahama), Kyela (Kyela), Vunjo (Vunjo) na Kayanga (Karangwe).
“Majimbo yote haya mengi ni ya CCM na ile dhana kwamba Chadema ni chama cha ukanda mmoja sasa uchaguzi huu umedhihirisha kwamba Chadema ni chama cha nchi nzima, kipo kila kona na hili halina ubishi tena,” alisema Dk. Slaa.CHANZO MWANANCHI

No comments:

Post a Comment