Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaanza mkutano wake wa 18
leo, ambao pamoja na mambo mengine, wabunge wanatarajia kuhoji
utekelezaji wa serikali wa maazimio nane ya Bunge kuhusu kashfa ya
kampuni ya IPTL ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kifisadi katika
akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Maazimio hayo yaliyopitishwa na Bunge Zima, Novemba 29, mwaka jana,
yalifuatia taarifa maalumu iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu ukaguzi maalumu wa malipo
yaliyofanyika katika akaunti hiyo.
Ukaguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru).
Taarifa hiyo ya PAC, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Zitto
Kabwe, bungeni, Novemba 26, mwaka jana, ilieleza kuwa mmiliki wa kampuni
ya Pan African Power Solutions Ltd (PAP), Harbinder Singh Sethi,
mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering & Marketing (VIP), James
Rugemalira, walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha
kufanyika miamala haramu ya fedha katika akaunti hiyo kwenda kwa kampuni
hizo.
Wengine waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kuhusika katika kashfa
hiyo, ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi,
Eliakim Maswi na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo aliyetajwa na PAC kuwa dalali kati ya Rugemalira na Sethi
kufanikisha uchotwaji wa fedha hizo.
Wamo pia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Frederick Werema na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco).
Hivyo, Bunge likaazimia kuwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine
husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria kwa
mujibu wa sheria za nchi watu wote waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC
kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya akaunti
hiyo na wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya PAC, vitendo vilivyofanywa na watu
hao vinaashiria makosa mbalimbali ya jinai, kama vile uzembe, wizi,
ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka,
rushwa na kupokea mali ya wizi.NIPASHE


No comments:
Post a Comment