Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Deo Filikunjombe wakiwa katika majukumu yao.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dk. Kamugisha Kazaura (kushoto) akiwa katika majukumu.
…………………………………………………………………………………………………..
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) imetoa mapendekezo ya kuinusuru Kampuni ya Simu Tanzania
(TTCL) kutokana na hali mbaya ya kampuni hiyo kifedha kwa sasa ambapo
inaendeshwa kwa hasara huku ikiwa na madeni makubwa.
PAC imetoa mapendekezo hayo katika
taarifa yao kwa bunge ya mwaka juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa
mashirika ya umma iliyotolewa Januari 28 mwaka 2015. Kwa mujibu wa
taarifa ya PAC hali ya mapato na matumizi ya TTCL kwa mwaka 2012 ilipata
hasara ya bilioni 20.883 huku kwa mwaka 2013 ikipata hasara ya bilioni
16.258.
PAC ilisema majumuisho ya hasara
ya TTCL kupata hasara kwa takribani kwa miaka 10, Kampuni sasa imekuwa
na hasara ambayo kwa mwaka 2013 ilifikia bilioni 334.48, jambo ambalo
limeiondolea mvuto wa kukopeshwa na taasisi za fedha hata zile zenye nia
ya kuikopesha.
“…Ukosefu wa fedha za kutosha
kutekeleza miradi ya Kampuni umekuwa kikwazo kwa TTCL kukabiliana na
ushindani wa kibiashara. Kwa kipindi kirefu ufanisi wa TTCL kiuwekezaji
na kifedha umeendelea kudorora. Tangu TTCL ibinafsishwe mwaka 2001,
hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika na mpango wa kutafuta mkopo kutoka
mabenki ya ndani na nje ya nchi unakwamishwa na masharti ya kupata
udhamini wa Serikali,” ilieleza taarifa hiyo ya PAC.
PAC iliongeza kuwa ukiacha madeni
yaliopo pia TTCL inadaiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
Tanzania (TCRA) jumla ya bilioni 25 hivyo kufanya jumla ya deni kufikia
bilioni 101.6. Kamati hiyo ya bunge imesema kuna umuhimu wa Serikali
kufanya maamuzi ya haraka ya kuikwamua TTCL ili iweze kuendelea kutoa
huduma kwenye Sekta ya Mawasiliano ikizingatiwa kuwa ndiyo inayoendesha
Mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
Katika mapendekezo ya PAC ili
kuikwamua TTCL imeishauri Serikali kununua hisa asilimia 35
zinazomilikiwa na Bharti Airtel katika TTCL kwa gharama ndogo kwani
Bharti Airtel haikutimiza kikamilifu masharti ya mkataba wa mauziano ya
hisa hizo hapo awali kwani tangu inunue hisa hizo haijafanya uwekezaji
katika Kampuni ya TTCL.
“…TTCL isamehewe deni la Serikali
Sh. 76.6 bilioni na deni la TCRA Sh. 25 bilioni ambayo jumla yake ni
Sh. 101.6 bilioni na fedha hizo zipelekwe kuongeza mtaji ili Kampuni
itoke kwenye kuwa na mtaji hasi wa Sh. 87.896 bilioni na kuwa na mtaji
chanya wa sh. 13.704 bilioni. Likifanyika hili basi Kampuni hiyo itaweza
kukopesheka.
Serikali ikamilishe taratibu zake
za kuimilikisha TTCL Mkongo wa Taifa ili izidi kuuendeleza kwa ufanisi
na kuongeza mapato ya TTCL,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. Hata hivyo
PAC imeshauri kuwa kuna umuhimu wa kufanya marekebisho ya muundo wa
Kampuni ya TTCL kwani kwa sasa ina idadi kubwa ya wafanyakazi (1549)
isiyoweza kuwalipa.
Aidha, ilibainisha kuwa kwa sasa
zinahitajika bilioni 32 kwa ajili ya kugharamia urekebishaji wa muundo
wa Kampuni ili uendane na mahitaji ya utoaji wa huduma mbalimbali.
Mashirika mengine yenye hali
mbaya kifedha na uendeshaji ni pamoja na Shirika la Ndege Tanzania, ATCL
ambayo kwa sasa ina madeni makubwa huku ikiwa na ndege moja aina ya
Dash 8–Q 300, Wafanyakazi 142 na Jengo la ATC House lililoko mtaa wa
Ohio, Dar es Salaam.


No comments:
Post a Comment