
KUTOKANA na wahalifu waliopambana juzi na polisi na Jeshi la Wananchi
(JWTZ) kutokamatwa, hali ya wasiwasi imeendelea miongoni mwa wakazi wa mjini
hapa.
Sasa wananchi hao wameiomba Polisi kutoa tamko, kuhusu kikundi
kilichorushiana risasi na askari Polisi na kusababisha kifo cha mwanajeshi
mmoja.
Aidha, wananchi hao wameitaka Polisi kutoa ufafanuzi kuhusu mwendelezo
wa matukio mengi ya uhalifu wa kutumia silaha, ambayo bado hayajapatiwa
ufumbuzi, ikiwemo kutokamatwa kwa watuhumiwa wa matukio hayo.
Hata hivyo, Msemaji wa Polisi, Advera, alisema Jeshi lake halina taarifa
zaidi ya iliyotolewa juzi na Mkuu wa Opersheni wa jeshi hilo, Kamishna Paul
Chagonja.
Habari za kipolisi zinasema kwamba bado wanaendelea kusaka wahalifu hao
huku baadhi ya vikosi vya ulinzi na usalama, vimeongezwa kwa ajili ya kupambana
na wahalifu hao. Juzi Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Polisi
walipambana na kundi la wahalifu katika maeneo ya mapango ya Amboni na
kusababisha wanajeshi wanne na polisi wawili kujeruhiwa.
Hata hivyo, kuna habari kuwa majeruhi mmoja ambaye ni mwanajeshi
alifariki baadaye akiwa hospitalini. Habari zingine zinasema kwamba majeruhi
wengine ambao ni polisi wanne na mwanajeshi mmoja, wanaendelea vizuri.
Kuhusu mwanajeshi aliyekufa, polisi wamegoma kuzungumzia suala hilo,
lakini habari zinasema aliyekufa ni mwanajeshi mwenye cheo cha sajenti.
Wananchi wametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti jana, walipozungumzia tukio la
juzi, lililosababisha mapigano ya kurushiana risasi baina ya askari na
wahalifu, wanaodaiwa kuficha silaha katika eneo la Mapango ya Amboni, nje
kidogo ya mji wa Tanga.
Walisema mpaka sasa bado hawajaridhishwa na mwenendo wa utendaji wa
Jeshi la Polisi mkoani hapa, pamoja na taarifa hafifu wanazotoa, kuhusu namna
walivyoshughulikia tukio hilo la juzi kwenye mapango hayo ya Amboni.
Ibrahim Mshote, mkazi wa Ngamiani Kati, alisema mbali na tukio la juzi,
yapo matukio mengine yakiwamo yaliyosababisha mauaji kwa raia, ambao walivamiwa
na kuporwa mali na watuhumiwa kushindwa kupatikana. Alisema hakuna taarifa za
mwendelezo wa kushughulikiwa kwa matukio hayo.
“Kwa mfano kuna wananchi walilipuliwa na bomu la kutupwa kwa mkono
wakati wakitazama mpira kwenye kibanda cha video hapo Amboni… pia yupo
mfanyabiashara wa eneo la Mkumbara wilayani Korogwe ambaye hivi karibuni
alivamiwa na kuuawa kwa risasi kabla ya kuporwa mali, pia tukio la utekaji wa
gari eneo la Michungwani wilayani Handeni baada ya kuwekewa magogo barabarani”,
alisema.
Aliongeza “Katika matukio kama hayo, tunaambiwa tu wahalifu
hawakupatikana, upelelezi unaendelea, lakini ni zaidi ya wiki mbili sasa hakuna
taarifa zozote zinazoonesha juhudi za mwendelezo wa kudhibiti wahalifu kama
hao, badala yake matukio yameendelea kuongezeka”.
Miriam Jonas, mkazi wa Barabara ya Tano jijini Tanga, alisema kitendo
cha askari kunyang’anywa silaha mbili za SMG zenye risasi 60 kwenye kibanda cha
chipsi ni fedheha kwa kuwa vitendo hivyo vilishasahaulika mkoani hapa.
“Tulitarajia wahusika wangekamatwa ndani ya muda mfupi, lakini wapi,
Polisi hapa Tanga imeshindwa kabisa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo hadi
Kamishna Chagonja alipokuja na kuzungumzia tukio la juzi”, alisema.
Aidha, Mrisho Mashaka mkazi wa Kwaminchi alisema licha ya Chagonja
kuwataka wakazi wa jiji la Tanga kutulia, kwakuwa hali ya usalama imeimarishwa,
bado baadhi ya wananchi wanayo shaka na hofu kubwa kuhusu tamko hilo.HABARI LEO


Watu mlio nje ya Tanga ndo mna hofu kubwa zaidi kuliko tuliomo huku. Watu tunaendelea na shughuli zetu kama kawaida.
ReplyDelete