Basi la Nganga linalofanya kazi zake kati ya Mbeya na Morogoro likiwa
linawaka moto mara baada ya kugongana na lori. Picha na mtandao
Morogoro. Watu 18 wameteketea kwa moto baada ya basi la Kampuni ya Nganga Express na lori aina ya Fuso kugongana uso kwa uso na kuwaka moto katika eneo la Iyovi, Milima ya Uduzungwa, Morogoro
Katika ajali hiyo iliyotokea jana saa mbili
asubuhi, abiria 15 waliokuwa kwenye basi na wengine watatu wa lori
waliteketea kwa moto huku wengine 10 wakijeruhiwa vibaya.
Taarifa na picha za ajali hiyo zilianza kusambaa
jana asubuhi kupitia mitandao ya kijamii zikionyesha masalia ya miili ya
walioteketea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul
alisema ajali hiyo ilitokea baada basi hilo lililokuwa linatoka
Kilombero kwenda Mbeya likiwa kwenye mistari ya barabarani ya katazo na
kwenye mwendo kasi kugongana na lori lililokuwa limebeba matikiti na
kuwaka moto.
Alisema majeruhi wanne wamelazwa katika Hospitali ya St. Kizito, Mikumi na sita wako katika Hospitali ya Mtandika, Iringa.
Alisema kwenye basi hilo kulikuwa na pikipiki ambayo pia iliungua na kusema inawezekana ndiyo iliyosababisha moto huo.
Ajali hiyo ni mfululizo wa ajali zinazotokea
katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni siku moja baada ya watu watano
kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mikoa ya Dodoma na
Iringa saa 36, baada ya kumalizika mgomo wa madereva nchini.MWANANCHI


No comments:
Post a Comment