
WAWAKILISHI wa pekee Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho, timu ya Yanga leo itakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha inapata sare au ushindi dhidi ya wapinzani wao, FC Platinum ya Zimbabwe ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Yanga itashuka kwenye uwanja wa ugenini wa Mandava kuvaana na wenyeji wao katika mchezo wa marudiano, huku ikiwa na mtaji wa mabao 5-1 walioupata katika mchezo wa awali uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo inayoongoza Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa na pointi 40, imeondoka nchini jana kwa ndege ya kukodi ya Serikali, ikiwa na asilimia kubwa ya kusonga mbele kutokana na ushindi mnono walioupata.
Kikosi cha vinara hao wa Ligi Kuu kilitua salama na kufikia kwenye Hoteli ya Rainbow jijini Bulawayo, kabla ya kusafiri kwa basi kwenda Gweru umbali wa takriban kilometa 200 kutoka Bulawayo.


No comments:
Post a Comment