![]() |
| Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (Ewura), Felix Ngamlagosi Serikali itaanza kuitumia Bandari ya Tanga kuingiza mafuta ifikapo
Julai Mosi, mwaka huu, kwa lengo la kupunguza msongamano katika bandari
ya Dar es Salaam.
Sababu nyingine ni kuinua uchumi wa mkoa wa Tanga pamoja na uharakishaji wa usafirishaji.
Aidha, waingizaji wa mafuta watakaotumia bandari hiyo watatumia
gharama ndogo tofauti na kutumia bandari ya Dar es Salaam huku fedha
zitakazopatikana zikiingia kwenye mfuko wa kuboresha bandari ya Tanga.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (Ewura), Felix
Ngamlagosi (pichani), katika mkutano na wadau wa mafuta ambao uliokuwa
unajadili namna ya upangaji bei ya nishati hiyo kupitia bandari ya
Tanga.
Alisema mwaka 2012 kulikuwa na mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja
ambao kwa kiasi kikubwa ulisaidia kupunguza gharama za uingizaji mafuta
nchini na ukusanyaji kodi, akisisitiza kuwa imefikia wakati wa kutumia
bandari hiyo kwani meli nyingi zinashusha mafuta bandari ya Dar es
Salaam.
“Serikali imeamua kufungua bandari ya Tanga ili kupunguza
msongamano katika bandari ya Dar es Salaam pamoja na ucheleweshaji wa
kupakua shehena za mafuta bandarini kwani utakuta mafuta yanachelewa
mwezi mzima hivyo kusababisha gharama,” alisema.
Aidha, alisema haipendezi waagizaji wa mafuta kutumia bandari moja
kuingiza mafuta na kuwa ikiwa Taifa litatumia bandari zaidi ya moja
itasaidia kuharakisha usafirishaji wa nishati hiyo katika maeneo
mbalimbali ya nchi na kukuza uchumi.
Ngamlagosi alisema mfumo huo utasaidia nchi kushindana vyema
kibiashara na bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji) na Afrika
Kusini na kuliingizia Taifa kipato kupitia wafanyabiahara wa nje
wanaotumia bandari ya Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa mchakato wa ukusanyaji maoni ya wadau wa mafuta
ulifunguliwa Mei 19, mwaka huu huku ukitarajiwa kufungwa Juni 19, 2015.
Mwenyekiti wa Baraza la Walaji (Ewura CC), Prof. Jamidu Katima.
alisema kuwa kazi kubwa ya baraza hilo ni kuwatetea watumiaji wa
nishati hiyo.
“Tunaambiwa meli za mafuta zikishusha katika banadari ya Tanga
zitapunguza gharama kwa watumiaji hivyo tunapaswa kuliona hilo
likitendeka,” alisema.
Prof. Katima alisema kwamba ikiwa mafuta yatakuwa yakishushwa
katika bandari hiyo kwa bei nafuu ni wazi kuwa gharama za mafuta kwa
watumiaji wa mikoa ya jirani na mkoa husika zitakuwa chini.
|
June 18, 2015
BANDARI YA TANGA KUTUMIKA KUINGIZA MAFUTA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment