![]() |
| Dk. Mwele Malecela,
Mgombea
urais anayeomba ridhaa ya kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk.
Mwele Malecela (pichani), amewataka Watanzania kutouza kura zao kwa
kuangalia fedha za muda mfupi.
Ameonya kuwa kwa kufanya hivyo, watasababisha nchi kupata viongozi ambao hawatawasaidia kutatua changamoto zao.
Dk. Mwele aliyasema hayo jana wakati anazungumza na wadhamini kwa
lengo la kuwashukuru, baada ya kumdhamini katika mkoa wa Kusini Unguja,
visiwani Zanzibar.
Dk. Mwele alisema kuwa Watanzania wakichagua viongozi kwa sababu ya
kupewa fedha watashindwa kuwawajibisha au kuhoji juu ya utendaji wao wa
kazi pale wanapokwenda kinyume cha maadili ya uongozi.
“Watanzania tuwe makini kipindi hiki cha uchaguzi, unapochagua
viongozi kwa kupewa fedha ujue siku ukimuelezea matatizo yako atakwambia
tulishamalizana tangu kabla ya uchaguzi nilishakupa chako,” alisema.
“Kiongozi wa namna hiyo anaona kuwa kipindi cha kampeni alipokuwa
akitoa fedha alikuwa anawalipa kwa kipindi atakachokaa madarakani ili
afanye mambo yake na hatutaweza kumuuliza chochote wakati huo,” alisema
Dk. Mwele.
Dk. Mwele alisema kuwa vipaumbele vyake vipo ndani ya ilani ya Chama na kwamba atavieleza akishateuliwa kupeperusha bendera.
Alisema: “Wagombea wengi wamekuwa wakitaja vipaumbele vyao sambamba
na kaulimbiu ila mimi nasubiri ilani kwa sababu siwezi kuahidi vitu
wakati sijajua kama vimo kwenye ilani nitawadanganya.” Pia Dk. Mwele
alisisitiza kudumishwa Muungano kwani ndio unaolitambulisha Taifa na
watu wake nje ya nchi.
Alisema kizazi kilichopo kimeukuta Muungano katika hali nzuri,
hivyo hakuna sababu ya kuwarithisha watoto wetu Muungano mbovu utakaozaa
chuki na uhasama baina yao.
“Mimi nimezaliwa ndani ya Muungano na nimekulia ndani ya Muungano
sijui chochote tofauti na Muungano kwa hiyo sina sababu ya kukitafuta
nisichokijua,” alieleza.
“Kutafuta muundo wa Muungano au mfumo wa nchi tofauti na uliopo
ambao tumeachiwa na waasisi wetu ni kutafuta tusichokijua, naomba
Watanzania wenzangu tuudumishe Muungano, maana ndio umoja wetu na amani
yetu,” alifafanua.
CHANZO:
NIPASHE
|
June 20, 2015
DK. MWELE MALECELA: MSIUZE KURA KWA KUANGALIA FEDHA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment