KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

June 17, 2015

KINANA: WANA - CCM IKOSOENI SERIKALI IKIKOSEA SIYO KUSIFIA TU.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.             
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amewataka wana-CCM kuikosoa serikali pale inapokosea badala ya kuisifu hata kwa mabaya.
 
Amesema kitendo cha kuisifia serikali hata inapokosea husababisha kukosekana kwa utendaji kwa viongozi walioko madarakani.
 
"Serikali inakosea na ni wajibu wa CCM kuikosoa badala ya kusubiri wapinzani waandamane na kufanya hivyo ni kuongeza utendaji wa viongozi na watendaji walioko serikalini," alisema.
 
Kinana aliyasema hayo juzi wakati akihutubia wananchi wa Wilaya ya Chato kwenye viwanja vya kituo cha mabasi cha zamani baada ya kuanza ziara ya siku saba mkoani Geita akitokea mkoani Kagera.
 
Alisema hakuna sababu wala faida ya kuisifu serikali ambayo kila mara inaboronga hali ambayo inasababisha wananchi kukichukia chama hicho kwa sababu ndicho chenye serikali.
 
"Lazima wana-CCM tujifunze kuikosoa serikali, haiwezekani kila mara tuwe na kazi ya kuisifia tu hata kama ikikosea, serikali ni ya chama chetu, hatuwezi kusifia maovu na pale serikali itakapofanya vizuri tutaisifia," alisema Kinana.
 
Alisema hakuna serikali inayoomba kura isipokuwa chama ndicho kinaingia dhamana na wananchi wakati wa kuomba ridhaa ya kuwatumikia.
 
"Wakati tunaomba kura, hawa watendaji wa serikali wanakuwa wametulia hawana habari, sisi ndiyo tunatumia nguvu kubwa kuomba ridhaa, tunapochaguliwa ndiyo tunachagua watendaji wa kufanya nao kazi tunapounda serikali,  hivyo ni wajibu wetu kuikosoa," alisema Kinana.
 
Kwa upande wake, Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema mwaka 2012 waliweka maazimio ya kukitoa chama ofisini na kukipeleka kwa wananchi, hali ambayo imekifanya kiimarike.
 
Alisema chini ya Katibu Mkuu wake Kinana, wamefanya mambo makubwa ikiwamo kuwafikia wananchi na kukifufua Chama kwani kilishapoteza mwelekeo pamoja na kuikosoa serikali.
 
"Wana-CCM tuna kila sababu ya kutembea kifua mbele, Kinana amefanya kazi kubwa sasa Chama kinaheshimika na ushindi 2015 ni lazima, hatuna shaka na dereva tuliyenaye," alisema Nape

No comments:

Post a Comment