![]() |
| Askari wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mwenzao, William Mtika
aliyeuawa kwa kupigwa risasi na majambazi juzi walipopambana katika
tukio la uporaji mali na fedha eneo la Iwambi jijini Mbeya. Mwili huo
umesafirishwa kwenda mkoani Mara kwa mazishi. Picha na Godfrey Kahango.
Mbeya. Majambazi yamemuua polisi wa upelelezi, William Mtika
(29) wa jijini hapa wakati wa mapambano kwenye tukio la kutaka kupora
fedha za Kampuni ya Export And Trading eneo la Iwambi.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:00 alasiri na
katika mapigano hayo, jambazi mmoja alipigwa risasi mguuni na baadaye
kufariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa marehemu
huyo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi alisema Mtika akiwa na
askari wenzake walipata taarifa za watu waliotiliwa shaka nyendo zao
eneo hilo ndipo wakaelekea kwenye tukio.
“Askari wakiwa eneo la tukio walifanikiwa
kuwakamata majambazi waliokuwa kwenye pikipiki baada ya kugonga gari la
Polisi kabla ya nyingine kutokea na kuwapiga risasi ambazo moja ilimpata
askari wetu Mtika,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Mnasa aliwataka
polisi kutorudi nyuma katika mapambano, huku akiwasisitiza wananchi
kutoa taarifa za watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao.
Mwili wa marehemu Mtika uliagwa jana mchana
nyumbani kwake eneo la Ghana Mbeya na kusafirishwa kwenda mkoani Mara
kwa ajili ya mazishi.Alisema polisi pia walifanikiwa kukamata bastola
moja iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za Shotgun na pikipiki
mbili.
Akifafanua chanzo cha tukio alisema, awali
majambazi walimvamia mfanyakazi wa kampuni aitwaye Madhu Basavaranjappa
lakini alipiga risasi juu ambazo ziliwafanya nao wajibu na hatimaye
kuamua kukimbia na ndipo walipokutana na polisi.
Kamanda Msangi alisema wanaendelea na msako mkali
wa kuwatia nguvuni majambazi hao huku akisisitiza kwamba kifo cha polisi
wake katu hakitawavunja moyo polisi bali kitaongeza morali kuhakikisha
wanapambana na aina yoyote ya uhalifu.
|
June 12, 2015
MAJAMBAZI YAUA POLISI MPELELEZI MBEYA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment