![]() |
| Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, jana alichukua fomu
ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), akisema hakuupata wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa (UN), kwa kupewa kama zawadi au urafiki, isipokuwa
alikidhi vigezo vya kiongozi aliyetakiwa kutoka Bara la Afrika.
“Ilikuwa ni zamu ya Afrika na ilikuwa lazima atoke Tanzania, bahati
ikawa kwa Asha-Rose, lakini si kama inavyofikiriwa kwamba kuna urafiki,
zawadi au hisani ilitolewa ndio nikaipata. Uongozi katika UN unapitia
mchujo, unachunguzwa kwa muda mrefu na wala hakuna kupewa kazi kwa
ujamaa,” alisema Dk. Migiro.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya CCM Mjini
Dodoma jana alasiri baada ya kuchukua fomu, Dk. Migiro alisema
alichaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutokana na
uwezo wake pamoja na sifa alizonazo; ndio maana Katibu Mkuu wa Umoja
huo, Ban Ki-Moon, alimkubali pasipo shaka.
Waziri Migiro alisema uamuzi alioufanya wa kutangaza nia ya
kugombea urais, unatokana na CCM kupanua wigo wa demokrasia kwa
kuwawezesha wanachama wengi zaidi kujitokeza katika mchakato wa
kumtafuta kiongozi muhimu wa Taifa.
“Mazingira mazuri na mafanikio yaliyojengwa na kufikiwa na CCM
katika awamu zote nne, yamenisukuma mimi kuwa mwanamke wa tatu kutangaza
nia ya kugombea nafasi ya urais, kati ya makada wengine 32
waliotangulia; nafarijika sana na wigo wa demokrasia uliopo,”
alisisitiza.
Kuhusu vipaumbele vyake akiteuliwa kuwa mgombea urais, Dk. Migiro
alisema: “Nasubiri ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoandaliwa ili
niitumie kama nyenzo kuu ambayo itakuwa imetaja maeneo yote muhimu.”
Hata hivyo, Waziri Migiro alisema mafanikio yaliyofikiwa na
serikali ya awamu ya nne, yamechochea ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa
huduma za afya na hivyo kuongeza umri wa kuishi kutoka miaka 45 hadi 60.
Dk. Migiro aliondoka nchini, Januari 5, mwaka 2007 akiwa Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, baada ya kuteuliwa kuwa Naibu
Katibu Mkuu wa UN na kuhudumu hadi alipomaliza muda wake, mwezi Januari
mwaka 2014.
Baada ya kurejea nchini, aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu
ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Idara ya Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa.
|
June 16, 2015
MIGIRO ACHUKUA FOMU, ASEMA HAKUBEBWA UN.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment