![]() |
| Kada wa CCM, Ritha Ngowi akionyesha begi lenye fomu za kuomba kugombea
kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia chama cha CCM baada ya
kukabidhiwa makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma jana. Picha na Edwin
Mjwahuzi
Dodoma. Kada wa CCM, Ritta
Ngowi amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama kuwania urais katika
uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huu na kusema akifanikiwa ataanzisha
kituo kikubwa cha kuwahudumia wastaafu, walemavu, wasiojiweza na
vijana.
Kuchukua fomu kwa mwanamama huyo, kunafanya idadi
ya wanawake waliojitosa mbio za urais kufikia watano kati ya 39
waliochukua fomu hadi sasa.
Wanawake wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk
Asha-Rose Migiro, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR),
Dk Mwele Malecela, Balozi Amina Salum Alli na Monica Mbega.
Akizungumza jana, Ritta ambaye hakuongozana na
wapambe kama ilivyokuwa kwa makada wengine wanaowania nafasi hiyo,
alifika saa tatu asubuhi kuchukua fomu hizo.
Ngowi alisema yeye ni mtu anayependa kukaa, kufanya kazi na kusaidia jamii.
“Na katika suala zima la utendaji wangu, nimefanya kazi moja kwa moja na jamii, sijawahi kukaa ofisini,” alisema Ritta.
“Kama nikipata nafasi hii, nitaendeleza mazuri
yaliyofanywa na marais waliopita, lakini zaidi nikiweka mkazo kwenye
masuala ya elimu na kukuza uchumi,” alisema.
Alisema angependa kuona kila mwananchi anapata elimu na kusiwapo na mtu atakayekaa bila kuwa na shughuli halali ya kufanya.
“Lengo langu ni kuondoa hali ya Watanzania kukaa
bila kufanya kazi na vijana wasikae kwenye makundi yasiyo na tija,”
alisema Ritta.
Alisema pia ana lengo la kuanzisha kituo kikubwa
cha wastaafu, wasiojiweza, walemavu wasio na msaada na vijana wasio na
mazingira ya kuajiriwa.“Vijana hawa tutawahifadhi katika kituo
kitakachokuwa na maji, hospitali, shule na huduma mbalimbali,”
alisisitiza.
Kuhusu elimu, alisema kuna watoto wengi
wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya kukosa ada hivyo kama atapata
ridhaa ya kuongoza, atahakikisha Serikali inabeba jukumu la kuwasomesha.
“Nitaangalia suala la ujenzi wa vivuko katika maeneo yenye foleni kubwa kiasi cha kuathiri uchumi wetu,” alisema.
|
June 23, 2015
MWINGINE ACHUKUA FOMU ZA URAIS CCM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment