
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein
amesema mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa asilimia 90 ndiyo
uliomsukuma kuchukua fomu ya kugombea tena urais wa Zanzibar kwa tiketi
ya CCM.
Aidha,
ameahidi endapo atapewa tena ridhaa ya kuiongoza Zanzibar katika miaka
mitano mingine, atahakikisha Zanzibar inakuwa na maendeleo na mabadiliko
makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo za kiuchumi na utawala bora.
Aliyasema
hayo jana alipozungumza na viongozi wa CCM katika Ofisi Kuu ya CCM
Kisiwandui mjini hapa mara baada ya kukabidhiwa fomu ya kuwania nafasi
ya urais wa Zanzibar.
Alifafanua
kuwa utekelezaji wa ilani ya CCM na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
mkubwa na kuleta maendeleo ndiyo uliomshawishi kugombea nafasi hiyo kwa
kipindi cha pili sasa.
“Nimeamua
kuchukua fomu kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM kwa
sababu ya kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa ilani ya CCM
kwa asilimia 90,” alisema.
Akiyataja
baadhi ya mafanikio yake, alisema mara baada ya kuingia madarakani
alifanya kazi kubwa kuhakikisha taasisi zinazokusanya kodi zinasimamia
majukumu yake ambapo katika mwaka 2011 Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB)
ilikuwa ikikusanya jumla ya Sh bilioni 13.5 na sasa jumla ya Sh bilioni
39 zinakusanywa kwa mwezi.(VICTOR)


No comments:
Post a Comment