Manispaa ya Ilala imesema imezuia uzinduzi wa kampeni za Ukawa Jangwani kwa kuwa siku hiyo kutakuwa na shughuli nyingine ya CCM.
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia.
Siku chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kuzindua kampeni za mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli, katika
viwanja vya Jangwani, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam imezuia
kuzinduliwa kwa kampeni za mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward
Lowassa, katika viwanja hivyo.
Hatua hiyo imechukuliwa huku Ukawa wakisema wamehujumiwa ili wasizindue kampeni zao keshokutwa.
Manispaa hiyo imeeleza kuwa imechukua hatua hiyo kwa kuwa siku hiyo kutakuwa na shughuli nyingine ya CCM.
Lowassa ambaye anawakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) vya UDP, CUF na NCCR Magezi katika uchaguzi huo,
amezuiliwa kuzindua kampeni katika viwanja hivyo kwa madai kuwa uwanja
huo utatumiwa kwa shughuli nyingine na CCM.
Mwenyekiti mweza wa Ukawa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-
Mageuzi, James Mbatia, alisema zuio hilo la kutumia uwanja huo limo
kwenye barua waliyopelekewa na Manispaa hiyo juzi.
“Jambo la kushangaza ni kuwa, awali tuliomba kufanya kampeni zetu
uwanja wa Taifa, lakini tukazuiliwa. Sasa tumeomba kuzindulia viwanja
vya Jangwani walikofanyia wenzetu wa CCM, lakini pia tumenyimwa kwa
madai kuwa kuna wenzetu wameshaomba kufanyia hapo mkutano, lakini
Mgurugenzi wa Ilala ameshindwa kututajia ni chama gani kilicho omba,”
alisema Mbatia.
Alisema uamuzi huo umewatatiza kwa sababu wanashindwa kuuelewa na
kutafsiri kuwa ni matumizi mabaya ya dola dhidi ya CCM kwa kutumia
viongozi na watendaji wake kuzuia kampeni za Ukawa.
Mbatia alisema kabla Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadiki, alikaririwa na vyombo vya habari akivitaka vyama vya siasa
visivunje taratibu na sheria za uchaguzi.
Alisema pia Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, alitoa onyo kwa vyama vya siasa kufuata kanuni na
taratibu za kampeni ili kuepuka uvunjifu wa amani katika kipindi hiki
cha kampeni za uchaguzi mkuu hadi uchaguzi utakapofanyika
.
“Jambo la kusikitisha na ambalo linatugawa Watanzania, chama dola
CCM, kilivunja taratibu hizo kwa kuvuka muda wa kampeni hadi saa moja
kasoro usiku badala ya kumaliza saa 12 jioni, pia siku ya uzinduzi, Rais
Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alitumia lugha za matusi,
lakini yote hayo yalifumbiwa macho na Nec,” alisema Mbatia.
Alisema kanuni na sheria hizo za uchaguzi pia zilivunjwa kwa
kuongozwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete na kwamba hayo yote
wakati yakifanyika Polisi na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki
walikuwa katika viwanja hivyo.
MANISPAA YAZUNGUMZIA ZUIO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, alipoulizwa sababu
za kuzuia Chadema kuzindua kampeni zake katika uwanja huo, hakuwa
tayari kuzungumzia akidai yuko kikazi mkoani Arusha na kwamba Ofisa
Utamaduni wa Manispaa hiyo anakaimu wadhifa wake.


No comments:
Post a Comment