WAUMINI wa dini mbalimbali nchini wamehimizwa kuliombea taifa katika
wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu ili shughuli hiyo iweze kumalizika
kwa amani na utulivu. Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alihimiza
hayo kwenye ibada maalumu ya kuwekwa wakfu Askofu wa Kanisa la Moravian
Jimbo la Kusini, mchungaji Kenan Panja iliyofanyika mjini Tukuyu
wilayani Rungwe.
Dk Bilal alisema kwa kiasi kikubwa sala na dua za viongozi wa
madhehebu yote ya dini nchini zimesaidia kuleta baraka na kudumisha
utulivu na mshikamano nchini. Alisema viongozi wa serikali wamejipanga
vilivyo kuhakikisha zoezi la uchaguzi linafanyika kwa amani na utulivu
na kubainisha kuwa serikali itasimamia na kuhakikisha uchaguzi unakuwa
huru na wa haki.
“Nawaomba viongozi wa dini zote nchini kuhamasisha waumini wao
kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kutekeleza haki yao ya
msingi kikatiba, kwa kuchagua viongozi bora watakaoongoza taifa letu
katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Amani ni sharti la kwanza katika maendeleo ya wanadamu. Vitabu vya
dini zote duniani vinafundisha umuhimu wa amani kwa wanadamu. Yesu
Kristo alipofufuka na kukutana na wanafunzi wake kwa mara ya kwanza neno
lake la kwanza aliwaambia Amani iwe kwenu.
Hakutaja jambo lingile lolote. Alitamka hilo kwa kutambua kwamba
ndani ya Amani kuna kila kitu,” alisema. Dk Bilal alisema palipo na
amani pana maendeleo, ustawi, uchumi mzuri, furaha na upendo hivyo kama
taifa ni wajibu wa kila mmoja kudumisha amani, umoja na mshikamano
vilivyojengwa kwa muda mrefu chini ya misingi imara iliyowekwa na
waasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume.
Alihakikisha kuwa viongozi waliopewa dhamana watahakikisha Tanzania
inaendelea kuwa kisiwa cha amani, umoja na mshikamano akisema hata
maandiko matakatifu yanaelekeza kuwa Atukuzwe Mungu juu mbinguni na
duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.
Aliwasihi waumini wa dini zote kukataa mitego yote inayoweza kuwanasa
na kusambaratisha umoja wa taifa, hususani katika kipindi hiki cha
uchaguzi mkuu. Kwa upande wake Askofu i Panja alisema changamoto za
kimaisha zinazowakabili waumini ni mambo yanayohitaji mchango wa
viongozi wa dini kushirikiana na watawala wa taifa kutafuta ufumbuzi
kupitia umoja na mshikamano.



No comments:
Post a Comment