![]()  | 
| Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Martin Loibooki akiongea na wanakijiji wa Olosinoni wanaoshiriki zoezi la kuzima moto unaonendelea kuwaka Mlima Meru katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha jana. | 
![]()  | 
| Moto unaoendelea kuwaka Mlima Meru katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha. | 
![]()  | 
![]()  | 
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MOTO WAUNGUZA SEHEMU YA MLIMA MERU
Moto mkubwa umezuka mwishoni mwa 
wiki hii na kuunguza sehemu ya Mlima Meru katika Hifadhi ya Taifa ya 
Arusha. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo cha moto huo ni vitendo
 haramu vya urinaji wa asali ndani ya msitu wa hifadhi hiyo.
Wananchi wapatao 200 kutoka vijiji
 jirani vya Olosinoni na Kisimiri Juu wakishirikiana na TANAPA 
wamefanikiwa kuudhibiti moto huo ili usiweze kuleta madhara makubwa kwa 
binadamu hususan wageni wanaotembelea hifadhi kwa lengo la kupanda Mlima
 Meru.
Hadi sasa hakuna wageni 
waliodhurika na moto huo na tahadhari zote zimechukuliwa ili kudhibiti 
madhara zaidi kwa binadamu na shughuli za utalii ndani ya hifadhi.
Shirika la Hifadhi za Taifa 
linaendelea kuwatahadharisha wananchi juu ya vitendo vya kuingia ndani 
ya hifadhi bila kibali kwa shughuli ambazo zinaweza kuwa chanzo cha 
kuzuka kwa mioto hii ambayo husababisha uharibifu wa mazingira pamoja na
 kuharibu vyanzo vya maji.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa 
moto huo unadhibitiwa kwa haraka, TANAPA imeongeza nguvu kazi ya 
wananchi wakishirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuweza kuudhibiti
 moto huo.
Mwisho, taarifa kamili juu madhara
 yaliyosababishwa na moto huo itatolewa mara baada ya kukamilika kwa 
zoezi la kuzima moto na umma utaendelea kupewa taarifa ya maendeleo ya 
zoezi la uzimaji wa moto kila wakati.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
21.09.2015
dg@tanzaniaparks.com
www.tanzaniaparks.com







No comments:
Post a Comment