![]() |
MAMLAKA
ya Kudhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imesitisha kwa
muda usiojulikana leseni ya usafirishaji abiria ya kampuni ya mabasi ya
Muro (Muro Investment Co. Limited), kwa kutokidhi viwango vya kiufundi
na usalama.
Aidha,
Sumatra imeiagiza kampuni hiyo kuwasilisha kwa mamlaka hiyo mpango wa
utengenezaji magari yake, nakala ya cheti cha ofisa usafirishaji wa
kampuni pamoja na mkataba wake wa ajira, iweze kujiridhisha endapo
matakwa ya kanuni za ufundi, ubora na usalama yamezingatiwa na
kutimizwa.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Gilliard Ngewe, kampuni hiyo
ilijulishwa kuhusu uamuzi huo ambao utekelezaji wake unaanza leo kwa
mabasi yote ya Muro yanayosafirisha abiria kutoka Dar es Salaam- Arusha
na Dar es Salaam- Mwanza.
Kufuatia
maelezo ya Ngewe, mabasi hayo yamekuwa yakilalamikiwa na abiria kwa
kuharibika mara kwa mara pindi yawapo safarini, hivyo kushindwa kutoa
huduma ya usafiri kwa viwango vinavyotakiwa.
Alisema, “Inapotokea
mabasi yanayosafirisha abiria yanapata hitilafu za mara kwa mara na
kushindwa kuwapa abiria mabasi mbadala wakamilishe safari zao, mamlaka
inawajibika kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja
na kusitisha leseni ya usafiri kwa kampuni husika”.
Mkurugenzi
Mkuu huyo alisema, hatua iliyochukuliwa dhidi ya kampuni ya Muro
ilizingatia ushahidi uliotolewa na abiria waliofikisha malalamiko yao
kwa mamlaka hiyo, wakiwemo walioachwa wakihangaika njiani Septemba 17,
mwaka huu, kwa zaidi ya saa 15 bila kupatiwa suluhisho wala huduma za
kibinadamu.
Inaelezwa
abiria hao walikuwa wakisafiri kwa basi la Muro lenye namba za usaji
T51BQP, kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, lililoharibika katika eneo
la Chalinze mkoani Pwani saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:30 usiku, bila
wahusika kuwaeleza abiria chochote.
Mamlaka
hiyo pia ilieleza kuwa, abiria wa mabasi hayo yaendayo Mwanza yakitokea
Dar es Salaam wamekuwa wakikutwa na kadhia ya aina hiyo wawapo
safarini, ambapo mara kwa mara wamejikuta wakihangaika njiani pindi
yanapoharibika bila kupatiwa ufumbuzi wa haraka.



No comments:
Post a Comment