KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

April 20, 2016

KITUO CHA JEMOLOJIA KUENDELEZWA ZAIDI

jio1
Mkurugenzi Mtendaji, wa Chuo cha Jemolojia  cha Madagascar, Rasolonjatovo Adrianirina  akizungumza na Washiriki wa Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito- Arusha yaliyoanza  jijini Arusha tarehe 19 hadi 21 Aprili, 2016.
jio2
Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka akizungumza wakati wa Semina ya Mafunzo kutoka Chuo cha Jemolojia cha Madagascar iliyotolewa wakati wa Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito- Arusha yaliyoanza  jijini Arusha tarehe 19 hadi 21 Aprili, 2016.
jio3
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Dominic Rwekaza (kushoto) akiwa na Meneja Mradi wa Usimamizi Endelevu wa  Rasilimali Madini (SMMRP), Mhandisi  Idrisa Yahaya na Kiongozi wa Mradi     wa SMMRP wa Benki ya Dunia, Mamadou Barry       wakizungumza mara baada ya kuhudhuria  Semina ya Mafunzo kutoka Chuo cha Jemolojia cha Madagascar iliyotolewa wakati wa Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito- Arusha yaliyoanza  jijini Arusha tarehe 19 hadi 21 Aprili, 2016.
jio4
Mjiolojia kutoka Idara ya Madini, Asimwe Kafrika akizungumza wakati Semina ya Mafunzo kutoka Chuo cha Jemolojia cha Madagascar iliyotolewa wakati wa Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito- Arusha yaliyoanza  jijini Arusha tarehe 19 hadi 21 Aprili, 2016.
jio5
Washiriki wa Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito- Arusha yaliyoanza  jijini Arusha tarehe 19 hadi 21 Aprili, 2016 wakiwa katika Semina ya Mafunzo kutoka Chuo cha Jemolojia cha Madagascar iliyotolewa wakati wa Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito- Arusha yaliyoanza  jijini Arusha tarehe 19 hadi 21 Aprili, 2016.
……………………………………………………………………………………………………………..
Na Asteria Muhozya, Arusha
Imeelezwa kuwa, Serikali imeandaa mpango wa  kuhakikisha inakiendeleza Kituo Cha Jemolojia Tanzania (TGC) ili kiwe kituo Bora cha utoaji mafunzo ya uongezaji thamani madini nchini.
 Hayo yameelezwa na Meneja Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP), Mhandisi Idrisa Yahaya katika Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 19 hadi 21, Aprili, 2016.
Mhandisi Yahaya aliyasema hayo baada ya kuhudhuria semina ya mafunzo kuhusu madini ya Vito na  uzoefu yaliyotolewa na Wataalam waliobobea kwenye Sekta hiyo kutoka nchi ya Madagasca wakati wa Maonesho hayo.
Mhandisi Yahaya alisema kuwa, bado jitihada zinafanywa na Serikali kuwekeza zaidi katika Kituo hicho jambo litakalopelekea kufikia kiwango ambacho nchi ya Madagasca imefikia katika utoaji mafunzo mbalimbali katika sekta hiyo.
Aliitaja mipango hiyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa wakufunzi kutoka nje ya Tanzania, kukiunganisha Kituo cha TGC na vituo vingine  vya kimataifa duniani na ununuzi wa vifaa vya mafunzo.
“ Bado tunahitaji kuwekeza zaidi katika Chuo chetu ili kuweza kufikia hatua iliyofikia nchi ya Madagasca. Kuna mipango mingi imeandaliwa kwa ajili ya kituo hicho,” alisema Mhandisi Yahaya.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha TGC, Musa Shanyangi akieleza mipango ya kituo hicho  mara baada ya kuhudhuria semina hiyo alisema ni pamoja na kuanzisha  kozi  ya Jemolijia, usonara, kuongeza idadi ya wanafunzi  wanaosoma  kozi  ya lapidary kutoka wanafunzi 18 wa sasa hadi wanafunzi 36, kuanzisha maabara ya utambuzi wa madini ya vito na kuanzisha makumbusho ya madini ya vito na bidhaa za usonara.
Akiwasilisha uzoefu wa  Chuo cha Jemolojia cha nchini Madagasca (IGM) wakati  akitoa  mada kuhusu chuo hicho kwa washiriki wa maonesho hayo,  Mkurugenzi Mtendaji, Rasolonjatovo Adrianirina alieleza kuhusu mafunzo na huduma mbalimbali zinazohusu Chuo hicho ambacho  kinatajwa kuwa Chuo bora  kwa utoaji wa  mafunzo ya aina mbalimbali katika fani za Jemolojia Afrika.
Alisema kuwa, mafunzo yanayotolewa na Chuo hicho yapo katika vipindi tofauti kulingana na aina ya mafunzo yanayotolewa na hivyo kuwataka washiriki kuona umuhimu wa kukitumia chuo hicho kupata mafunzo kwa lengo la kuwezesha uongezaji thamani wa madini katika nchi husika.
Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), cha jijini Arusha, kilianzishwa ikiwa ni moja ya hatua  za Serikali za kutimiza malengo yaliyomo katika Sera ya Madini ya Mwaka  2009 yenye lengo la kuongeza  mchango wa Sekta ya Madini katika pato la Taifa na ajira kwa Watanzania kupitia Uongezaji thamani madini hapa nchini.
Aidha, mafunzo yanayotolewa na Kituo hicho ni pamoja na ukataji na ung’arishaji wa madini ya Vito ( Lapidary), utengenezaji wa  bidhaa za mapambo,  (Jewelry Design and Manufacturing) na uchongaji wa vinyago vya mawe  (Stone Carving).
Uongezaji thamani madini unalenga kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania watakaofanya kazi kwenye vituo vya kuongeza thamani madini huku wengine wakijiajiri na kuongeza mapato ya Serikali, hivyo kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa.
Kituo cha Jemolojia  kilianzishwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.

No comments:

Post a Comment