![]() |
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), mkoani Kigoma. |
![]() |
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Kapteni wa Meli ya MV Liemba ya namna inavyoendeshwa, mkoani Kigoma. |
Serikali imeliagiza Shirika la
Reli Tanzania (TRL), kupitia upya mikataba ya ununuzi wa vichwa vya
treni na mabehewa ili kubaini kasoro zilizojitokeza na kuchukua hatua
stahiki kabla ya maboresho ya reli ya Tanga-Moshi-Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani Kigoma
wakati akikagua miundombinu ya reli na kusissitiza nia ya serikali
kufufua reli ya kanda ya kaskazini ili kuimarisha huduma ya uchukuzi
katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
“Kama Serikali tumewekeza vya
kutosha katika TRL, hivyo tunawataka mfanye biashara itakayolipa nasi
tutahakikisha popote reli ilipo inatoa huduma iliyokusudiwa na kuchangia
kukuza uchumi wa nchi”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amewataka
wafanyakazi wa TRL kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kupata bidhaa
na abiria wengi wa kuwasafirisha nchini kote.
Amesema Serikali imedhamiria
kuliongezea nguvu TRL ambapo baadhi ya mitambo kutoka Kampuni Hodhi ya
Rasilimali za Reli (RAHCO) itakabidhiwa kwa shirika hilo hivyo kulitaka
kuwa na mpango madhubuti wa kufanya biashara na kurudisha hadhi ya
usafiri wa reli hapa nchini.
“Fanyeni bidii ili mpate mzigo wa
kusafirisha kutoka Tanga kwenda Moshi na Arusha ili kufikia lengo la
kubeba mzigo wa tani milioni moja kwa mwaka”, amesisitiza Waziri Prof.
Mbarawa.
Amezungumzia umuhimu wa TRL
kuafanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini
(TPA), ili kuongeza kasi ya huduma za uchukuzi nchini, kuongeza fursa za
ajira na kukuza pato la shirika na taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
TRL, Bw. Masanja Kadogosa amesema TRL imejipanga kutafuta masoko ndani
na nje ya nchi ili kuboresha huduma za uchukuzi na kukuza pato lake.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amekagua Meli ya MV Liemba na kuitaka Mamlaka ya Usimamizi wa
usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kuhakikisha meli za MV Liemba
na MV Mwongozo zinakaguliwa na kufanya kazi inavyostahili katika Ziwa la
Tanganyika.
“Tumieni fursa ya kuwa karibu na
nchi za maziwa makuu kufanya biashara ili meli zetu zipate mzigo wa
kutosha na kuongeza mapato kwa taifa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ambaye yupo katika
ziara mkoani Kigoma amewataka viongozi na wafanyakazi wa taasisi zilizo
chini ya wizara yake kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuibua fursa za
kiuchumi katika ukanda wa magharibi na hivyo kufufua miundombinu
itakayochochea uchumi wa mikoa ya magharibi mwa Tanzania yenye fursa
nyingi za kibiashara.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment