KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

April 27, 2016

UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI


U2U1 Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
…………….
Wanadamu wameumbwa kwa hulka na silika ya kuwa na uwezo wa kuwasiliana miongoni mwao, jamii wanamoishi, taifa na hata ulimwenguni ili waweze kutimiza nia na azma yao ya kuwasiliana.
Ili mawasiliano hayo yakamilike ni lazima yabebe ujumbe unaokusudiwa kufikishwa katika jamii.
Ujumbe huo ili uweze kumfikia mlengwa, ni lazima iwepo njia ya kuufikisha ujumbe huo kwa mlengwa ambao huwasilishwa kwa maandishi (magazeti), sauti (redio) na picha (TV) pamoja na mitandao ya kijamii kupitia huduma ya inteneti.
Vyombo hivyo vya habari vinahusisha wataalamu ambao kazi yao ni kuhakikisha jamii inapata ujumbe kwa wakati ili kuweza kujenga, kuboresha na kuimarisha maisha yao kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Vyombo vya habari hakika vimekuwa ndio macho na masikio ya wananchi ili kufikisha ujumbe unaohusu mambo mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya nchi.
Tunapoelekea siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Mei 2 na 3, maadhimisho hayo mwaka huu yataadhimishwa nchini Finland, ambapo wanahabari wote duniani wataungana kuwakumbuka wenzao waliofariki dunia walipokuwa wakitekeleza majukumu yao na kupanga mipango mipya ya namna watakavyoboresha kazi zao ziwe za ufanisi zaidi.
Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa ya dunia hii, nayo haipo nyuma katika suala la uwepo wa vyombo vya habari.
Ni dhahiri vyombo vya habari nchini vimekuwa kiungo muhimu katika kisaidia Serikali kutoa taarifa mbalimbali na ajira hatua ambayo imesaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.
Ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania inayoongoza kwa kuwa na vyombo vingi vya habari, hali ambayo ni msingi wa kuajiri watu wengi zaidi katika tasnia hiyo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ambaye ndiye mwenye dhamana ya habari nchini anasema Serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na vyombo vya habari nchini.
“Tulipofika ni pazuri ukilinganisha na tulipotoka, mengi yamefanyika hasa ukiangalia idadi ya vyombo vya habari nchini na uhuru wa waandishi wa habari wanavyoanadika na wanavyofikisha ujumbe kwa wasomaji, wasikilizaji na watazamaji” alisema Waziri Nape.
Aidha, Waziri Nape amesema kuwa bado Serikali inakusudia kuboresha mazingira ya waandishi wa habari ili waweze kufanya kazi zao kwa hali ya uhuru hasa wanapotimiza majukumu yao ya kiundishi wa habari.

No comments:

Post a Comment