Na Mwandishi
Wetu,
Wakulima wa zao la mpunga wanaojishughulisha kilimo
cha umwagiliaji katika Kijiji cha Mkula wilayani Kilombero wamefanikiwa
kupata mkopo wa 890Mn kutoka Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga.
Hayo yaliwekwa bayana na Mkurugenzi wa
Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal wakati wa warsha ya wakulima
wadogo zaidi ya 340 wa Mkoa wa morogoro iliyofanyika katika Ukumbi wa Mazingira
Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Bw. Paschal alisema lengo la mkopo huo
unaowanufaisha zaidi ya wakulima 350 ni kuongeza tija na uzalishaji wa mpunga
ili Kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu
nchini Tanzania na kuchagiza na
kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka
kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa
uchumi na kupunguza umaskini.
“Mkopo huu na mengine tunayotoa imelenga
kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo ili kusaidia kukabiliana na mapungufu
hayo na kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo ili kuleta
mapinduzi katika kilimo nchini,” alisema
Bw. Paschal.
Kwa mujibu wa Bw. Paschal mkopo huo utasaidia shughuli mbalimbali za utayarishaji
wa mashamba, kupima ubora wa udongo na virutubisho vinavyohitajika kwenye
uzalishaji wa mpunga pamoja na kuwezesha upatikanaji wa pembejeo za kilimo
zikiwemo mbegu bora, mbolea na madawa.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa Benki
imetoa mkopo kwa ajili ya uwekezaji kwenye
ujenzi viwanda vya kusindika mazao, ununuzi wa mitambo na ufungaji wa
mitambo ya usindikaji wa mpunga ili kuongeza thamani wa zao hilo.
“Tunaamini mkopo huu utachagiza kuongezeka
kwa upatikanaji wa chakula na Pato la Taifa kutokana kuongezeka kwa tija na
uzalishaji hivyo kuwa chachu ya ongezeko la thamani, ukuaji wa viwanda vya
mazao ya kilimo hivyo kuchangia kuongezeka kwa ajira nchini,” aliongeza.
Akizungumzia mikakati ya TADB kwa sasa, Bw.
Paschal alisema Benki imejipanga kutoa mikopo ya Muda Mfupi, Mikopo ya Muda wa
Kati na Mikopo ya Muda Mrefu kwa kutumia njia mbalimbali. Mbinu hizo zinajumuisha
pamoja na mambo mengine; mikopo ya moja kwa moja kwa vikundi vya wakulima
wadogo wadogo; kutoa mikopo kwa njia ya marejesho taasisi zinazokopesha; utoaji
wa mikopo kwa pamoja na kushirikiana na taasisi/benki zingine; pamoja na mikopo
ya miundombinu inayolenga kupunguza mapengo ya upatikanaji wa fedha katika
minyororo ya ongezeko la thamani ya kipaumbele.
“Kwa kuanzia, TADB imelenga uwekezaji katika
maeneo nane (8) ya minyororo ya uongezaji wa thamani ambayo ni: nafaka, kilimo
cha mboga mboga, kilimo cha bidhaa za viwanda, mbegu za mafuta, ufugaji wa
ng’ombe, ufugaji kuku, ufugaji wa samaki na bidhaa za misitu. Benki pia inajitahidi
kusimamia fedha kutoka kwa wafadhili wengine ambazo zimeelekzwa kwenye
kuendeleza kilimo,” alisema.
Warsha hiyo ilifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya
Kilombero, Mhe. Lephy Gembe ambaye alitoa rai kwa Wakulima wote waliopata fursa
ya kuhudhuria warsha hiyo kujipanga katika kuchangamkia fursa za mikopo
inayotolewa na TADB.
Mhe. Gembe zingatia mada zilizowasilishwa ili
waweze kunufaika na Benki hii na shughuli zinazotolewa na Taasisi zingine za
serikali
“Nawasihi mrudishe mikopo mtakayopewa kwa wakati
ili wakulima wengine waweze kunufaika zaidi na Benki hii na vile vile kuwezesha
Benki kutoa huduma kwenye maeneo mengine ya Tanzania,” alisema.


No comments:
Post a Comment