![]() |
| Rais Yahya Jammeh ameiongoza Gambia tangu 1994 |
Gambia inasema itajitoa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC baada ya kuishutumu kwa kuwa aibisha Waafrika.
Taifa hilo dogo la Afrika magharibi linajiunga na Afrika kusini na Burundi katika kutangaza kujitoa katika mahakama hiyo.Mahakama ya ICC iliundwa kusikiliza kesi mbaya zaidi duniani lakini imeshutumiwa kwa kuwalenga kwa njia zisizo za haki viongozi wa Afrika.
Waziri wa habari nchini Gambia Sheriff Bojang amesema mahakama hiyo imepuuza uhalifu wa kivita wa mataifa ya magharibi.
Amesema ICC, kwa mfano imeshindwa kumshtaki aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair kuhusu vita nchini Iraq.
Akizungumza kwenye televisheni, amesema ICC, ni mahakama ya 'watu weupe wenye nywele za singa ya kuwashtaki na kuwa aibisha watu wasio weupe, zaidi Waafrika'.
Mwendesha mashtaka mkuu katika mahakama hiyo, Fatou Bensouda, alikuwa waziri wa sheria Gambia.
Rais Yahya Jammeh ameitawala Gambia tangu alipoingia madarakani kupitia mapinduzi mnamo 1994.
Uchaguzi unatarajiwa Desemba, lakini kiongozi wa upinzani Ousainou Darboe na wengine 18 wamefungwa kwa miaka 3 maema mwaka huu kufuatia maandamano ynayaosemekana kuwa ya haramu.
Nchi hiyo imekuwa ikijaribu kuushtaki Umoja wa Ulaya katika mahakama ya ICC kufuatia vifo vya maelfu ya wahamiaji wa Afrika wanaojaribu kuingia katika bara hilo kwa boti. BBC



No comments:
Post a Comment