Taasisi
ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imekaribisha uwekezaji zaidi kwenye
sekta ya Bima nchini ili kuibua ushindani utakaochochea ubunifu wenye
tija zaidi kwa wadau wa sekta hiyo.
Akizungumza
mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla fupi ya
uzinduzi wa kampuni mpya ya Bima ijulikanayo kama Clarkson Insurance
Brokers Tanzania Limited, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF , Bw. Godfrey
Simbeye alisema ustawi wa uchumi wa nchi kwa sasa unahitaji uimara na
ubunifu zaidi kwenye sekta ya bima hivyo wingi wa kampuni hizo unaweza
kuwa na tija zaidi katika kufanikisha hilo.
“Tanzania
kwa sasa ipo kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa kama ile ya bomba la
mafuta, ujenzi wa reli ya kati, ujenzi wa barabara na majengo makubwa ya
kisasa, vyote hivi vinahitaji kulindwa na bima hivyo ujio wa kampuni
kama hii ya Clarkson Insurance Brokers Tanzania Limited tunauona kama ni
heri na wenye tija kwa taifa,’’ alibainisha.
Kwa
mujibu wa Bw Simbeye kwa sasa mchango wa sekta ya Bima kwenye Ukuaji wa
Pato la Taifa (GDP) ni chini ya asilimia 1 huku akiitaja sekta binafsi
kuwa ni miongoni mwa sekta ambazo bado hazijafaidi ipasavyo matunda ya
uwepo wa huduma za Bima ambapo alitaja suala la ukosefu wa ubunifu
miongoni mwa makampuni ya Bima kuwa ni moja ya sababu ya uwepo wa
changamoto hiyo.
“Matumaini
yangu kwa kampuni ya Clarkson Insurance Brokers Tanzania Limited kwa
kiasi kikubwa yanachochewa na ukongwe wao wa miaka 58 wakitoa huduma hii
nchini Kenya ikiwa ni pamija na Uganda hivyo natarajia kwamba uzoefu
wao katika kipindi hicho kirefu unaweza kuwa na tija zaidi hapa
nchini,’’ aliongeza.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa makampuni ya Bima ya Clarkson Insurance
Brokers Tanzania Group Bw Justin Lambert alisema pamoja na kutoa huduma
kwa weledi, kampuni yake itajikita zaidi katika kutoa elimu ya bima kwa
jamii ili kuwavutia zaidi wengi ambao kwasasa bado hawajaingia kwenye
huduma hiyo.
“Clarkson
Insurance Brokers hatujaingia hapa nchini ili kuongeza idadi ya
makampuni ya bima yaliyopo nchini bali lengo letu hasa kuongeza
ushindani na kuleta mapinduzi makubwa na yenye tija kwa wadau wa sekta
hii muhimu,’’ alibainisha.
Nae,
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo hapa nchini Bw, Patrick Marimo
alisema mafanikio ya kampuni hiyo katika soko lake jipya hapa nchini kwa
kiasi kikubwa yatachochewa na ubunifu mkubwa wa kampuni hiyo katika
utoaji wa huduma zake.
“Tunalenga
kuleta mabadiliko makubwa kwenye huduma hii muhimu na ndio maana pamoja
na mambo mengine tutajikita zaidi katika kutoa elimu kwa jamii ili
kuijengea uelewa zaidi kwenye masuala ya bima ili tutoe huduma kwa watu
wenye uelewa zaidi …lakini pia uwekazaji wetu kwenye teknolojia ya
kisasa unaweza kuwa chachu zaidi katika kufikia malengo,’’ alisema.

Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Kampuni ya Clarkson Insurance Brokers inayojishughulisha na masuala ya bima Bw. Godfrey Simbeye
ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF akionyesha zawadi aliyokabidhiwa
na Mwenyekiti wa Kampuni ya Clarkson Insurance Brokers Justin Lambert
mara baada ya uzinduzi wa kampuni hiyo uliofanyika kwenye hoteli ya
Hyyat Kilimanjaro Kempinski jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki.


No comments:
Post a Comment