Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza viongozi wote wa Serikali
walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru
kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Wilaya ya Bariadi
Mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao walishalipwa fedha
ya posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe
Taarifa iliyotolewa leo tarehe 12
Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
John Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli ametoa maagizo hayo ikiwa ni
utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi
yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za
maendeleo ya nchi.
Viongozi waliotajwa kutakiwa
kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na Wakuu wote wa Mikoa,
Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Mameya na Wenyeviti wote wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na
Wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao wakiwemo madereva na
wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.
Kwa kuwa sherehe za Kilele cha
Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu
ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere aliyefariki dunia miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka
Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na
kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.
Aidha, Rais Magufuli ameagiza
Wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati
Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi
katika siku ya kilele cha Mbio za Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa
zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka
inayohusika kutoa zawadi hizo.
Hata hivyo Dkt. Magufuli
ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa,
Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na Wilaya zake pamoja na
wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika
sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016.
Mgeni Rasmi katika sherehe za
kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Oktoba, 2016


No comments:
Post a Comment