Na Jonas Kamaleki, MAELEZOShilingi bilioni 374.5 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya nyumba hapa nchini ili kuwawezesha wanachi kuwa na makazi bora ambayo ni haki ya msingi ya kila mwanadamu.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani.
“Ili kukidhi mahitaji ya nyumba yanayotokana na ongezeko kubwa la watu, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeshiriki katika utoaji wa mikopo ya nyumba ambapo soko la mitaji na mikopo ya nyumba nchini limeongezeka na kufikia asilimia 6.7 kwa mwaka jana,”alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, taarifa za Benki Kuu zinaonyesha kuwa idadi ya benki zinazotoa mikopo ya nyumba zimeongezeka kutoka tano kwa mwaka 2010 hadi kufikia 26 Desemba 2015.
Aidha. Lukuvi amesema kuwa utoaji wa mikopo ya muda mrefu ya nyumba umewezesha sekta binafsi na waendelezaji milki kuingia katika biashara ya kujenga na kuuza nyumba za biashara na makazi kwa kuwauzia wananchi kwa mkopo wa muda mrefu.
Aliongeza kuwa ili kuwezesha sekta ya nyumba kuendelea kufanya vizuri, Serikali inafanya mapitio ya sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya nyumba, zikiwemo Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000. Lengo la mapitio hayo ni kuweka mfumo wezeshi ambao utarahisisha uendelezaji wa sekta hiyo.


No comments:
Post a Comment