Wanafunzi
sita waliofanya vizuri sana katika mitihani wa taifa ya Kidato cha Sita ya mwaka
2016 na shahada ya kwanza wameshinda udhamini wa elimu ya chuo kikuu kwa mwaka
wa 2016/17 kupitia Mfuko wa Udhamini wa Elimu wa Kumbukumbuku ya Mwalimu Julius
Nyerere unaosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mwenyekiti
wa Kamati ya Udhamini ya Mfuko huo na Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Natu Mwamba
alisema katika taarifa yake kwamba kati ya hao sita, wanne ni wanafunzi wa kike
na wawili wa kiume, ambapo kati yao wanne watadhaminiwa kusomea shahada ya
kwanza na wawili shahada ya uzamili katika masomo ya science na hisabati.
Waliochaguliwa kudhaminiwa shahada
ya kwanza ni miongoni mwa wanafunzi bora 10 katika matokeo ya Mtihani wa Taifa
wa Kidato cha Sita kwa mwaka 2016, na watakaodhaminiwa shahada ya uzamili walipata
ufaulu juu wa Daraja la Kwanza katika mitihani yao ya shahada ya kwanza.
Dkt. Mwamba aliwataja waliochaguliwa
kozi za shahada ya kwanza watakaosoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa ni Bi.
Magreth Deusdedith Kakoko (Sayansi Uhandisi Ujenzi) Bi. Bertha Peter Nguyamu
(Sayansi Uhandisi wa Mafuta na Bw. Japhet Swema Lawrence (Biashara – Uhasibu). Bi.
Juliana Elias Mwalupindi (Uhasibu, Sekta ya Biashara) atasoma katika Chuo Kikuu
cha Mzumbe. Aidha, Bw. Shega Mayila na Bi. Elizabeth Elisey Mrema wanadhaminiwa
kusoma shahada ya uzamili (Sayansi – Hisabati) katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Mfuko wa
Udhamini wa Elimu wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere ulianzishwa na BoT
mnamo tarehe 12 Oktoba,
2009 kama njia ya kuenzi mafanikio makubwa ya Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere.
Lengo kuu la
Mfuko huu ni kuongeza hamasa na ufaulu kwa
wanafunzi wa kike hapa nchini katika masomo ya Hisabati na Sayansi. Mfuko
umejikita kutoa udhamini kwa wasichana wanaofanya vizuri katika mitihani ya
taifa ya Kidato cha Sita kuweza kusoma shahada ya kwanza kozi za hisabati na
sayansi katika vyuo vikuu hapa nchini.
Sehemu ya
udhamini huo hutumika pia kwa wanafunzi wa kike na wa kiume waliofanya vizuri
katika mitihani ya Kidato cha Sita kusomea shahada za uchumi, teknolojia ya
habari na mawasiliano (TEHAMA), uhasibu na fedha na wanafunzi wote wa kike na
kiume kusomea shahada ya uzamili katika masomo hayo.
Mfuko
ulianza kutoa udhamini 2013/14. Hadi hivi sasa jumla ya Watanzania 22 wamepata
udhamini huo; kati yao 16 ni wanawake na 6 ni wanaume. Baadhi yao
wamekwishamaliza kozi zao na kupata ufaulu wa juu na wengine wanaendelea na
masomo yao katika fani za Uhandisi-Mafuta na Gesi, Sayansi
ya Mafuta na Jiolojia, Udaktari, Ufamasia, Usanifu Majengo, Sayansi (Kemia),
Sayansi - Uchambuzi wa Masuala ya Bima (actuarial sciences), Uhasibu, Fedha,
Uchumi na Takwimu, TEHAMA na Uongozi.
Udhamini
unaotolewa chini ya Mfuko huu unahusu gharama zote za masomo zinazolipwa moja
kwa moja kwa vyuo vikuu husika na zile ambazo zinalipwa kwa wanafunzi kulingana
na mahitaji ya masomo yao. Aidha, kila mwanafunzi hupewa kompyuta mpakato
(laptop) kwa ajili ya kumsaidia katika masomo yake.
Aidha, tangu
mwaka 1994 BoT imekuwa
ikitoa udhamini ujulikanao kama Gilman Rutihinda Scholarships kwa
wanafunzi waliofanya vizuri katika shahada zao za kwanza kusoma shahada ya
uzamili. Hadi Februari mwaka huu, jumla ya wanafunzi bora 31 wamedhaminiwa
kusoma shahada ya uzamili katika masuala ya uchumi, fedha na biashara ya
kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Cha Usimamizi wa Fedha
(IFM).
Imetolewa na
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
03-10-2016



No comments:
Post a Comment