Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe Angellah Kairuki akijadiliana jambo na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt.Henry Mambo, katika moja ya hafla jijini Dar es Salaam hivi karibuni(Picha na Maktaba)
Na
Mwandishi Wetu
Chuo Cha Utumishi wa
Umma Tanzania (TPSC) kwa mara ya kwanza kimeanzisha Masomo ya Shahada ya kwanza
(Degree) katika fani za Uhazili na
Utunzaji wa Kumbukumbu, Taarifa na Nyaraka.
Kufuatia kuanzishwa
kwa masomo ya Shahada ya kwanza katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Mkuu
wa Chuo Dkt. Henry Mambo ametoa wito kwa watumishi wa umma na Watanzania wenye
sifa kuchangamkia nafasi hizo za masomo kwa manufaa yao binafsi na Taifa kwa
ujumla.
Dkt. Mambo alisema masomo
hayo ya Shahada ya kwanza yataanza Mwezi Septemba,2017 katika Matawi ya Dar es
Salaam na Tabora, nayo ni hatua kubwa kwa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania
katika kuwaendeleza Watumishi na Watanzania Kitaaluma.
Kwa upande wa sifa za
kujiunga na masomo hayo ya shahada ya kwanza, Dkt. Mambo alisema muombaji
anatakiwa kuwa na elimu ya kidato cha sita pamoja na ufaulu katika masomo
mawili au Diploma katika fani husika yenye ufaulu au GPA alama 3.
Mkuu wa Chuo pia
aliendelea kufafanua kwamba Masomo hayo ya ngazi ya Shahada yameanzishwa ili kuhakikisha kwamba watumishi
wa umma na Watanzania wenye sifa za kujiunga wanakabiliana na changamoto zinazojitokeza
katika soko la ajira kufuatia mabadiliko ya teknolojia na mifumo mbalimbali ya
utendaji kazi.“Kutokana na mabadiliko hayo ni vema Watumishi wa Umma na
Watanzania wenye sifa kwa ujumla nao wakapata mafunzo ambayo yatawawezesha
kukabiliana na changamoto mbalimbali katika soko la ajira,”.
Kuhusu shahada
ya Uhazili na Utawala, Mkuu wa Chuo alisisitiza
kwamba Wahitimu wataweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za
mawasiliano katika utendaji wao wa kazi wa kila siku na hivyo kuwawezesha kufanya
kazi kwa ufasaha katika sekta ya umma na hata sekta binafsi. “Mafunzo hayo pia
yatawawezesha wahitimu kumudu nafasi ya Maofisa Wasaidizi Waandamizi ambao
watafanya kazi katika taasisi mbalimbali hapa nchini na hata nje ya nchi kulingana na soko la ajira
litakavyowahitaji” alisema.
Kuhusu Shahada ya
Utunzaji Kukumbukumbu, Taarifa na Nyaraka, Mkuu wa Chuo cha Utumishi alibainisha kwamba mafunzo hayo yatawawezesha
wahitimu kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha mkubwa zaidi katika eneo hilo na
hivyo kuchangia katika uendelezaji na ukuaji wa Taaluma ya Utunzaji
Kukumbukumbu, Taarifa na Nyaraka.
Mafunzo ya ngazi ya
shahada (Degree) yatatolewa kwa muda wa miaka mitatu, wakati yale ya Diploma na
Cheti yataendelea kutolewa kwa kipindi cha miaka miwili na mwaka mmoja kama
kawaida na akatoa wito kwa watumishi wa umma na watu wote wenye sifa za
kujiunga na masomo hayo kuchangamkia fursa hizo kwa kujaza fomu za kujiunga na
Chuo zinazopatikana katika matawi yote ya Chuo cha Utumishi wa Umma ya Dar es Salaam, Tabora, Singida,Mtwara, Tanga
na Mbeya, na katika tovuti ya Chuo www.tpsc.go.tz
Katika kongamano la Mkutano
Mkuu wa mwaka wa Chama Cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) lililofanyika hivi
karibuni Mkoani Dododma, Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa kufungua
Mkutano huo, aliwataka makatibu Mahsusi hao kuichangamkia kozi hiyo, kwa kuwa ni fursa nzuri kwa Makatibu Mahsusi
na itawasaidia sana katika kuongeza
weledi na ufanisi kazini.
Nae Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angellah Jasmine Kairuki, ambae pia alihudhuria Kongamano hilo na ambaye Chuo
cha utumishi wa Umma kiko chini ya Wizara yake, aliwatoa hofu waombaji wa kozi
hizo mpya zilizoanzishwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kusema Ofisi
yake inalitambua hilo na inalifanyia kazi suala hilo ili Wahitimu
watakapomaliza mafunzo yao ya miaka mitatu(3), waweze kutambulika nafasi zao
katika Muundo wa Utumishi wa Umma. Hivyo akawahimiza Makatibu Mahsusi na
Watunza Kumbukumbu Taarifa na Nyaraka kuchangamkia nafasi hizo.
Mwandishi wa gazeti
hili pia aliweza kuongea na Katibu Mkuu wa TAPSEA, Festo Melikiory ambaye alisema kuwa kuanzishwa kwa kozi hizo
ni fursa kwa Watanzania hususan Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu na kwamba ni matumaini yake kuwa kozi hizo
zitaongeza weledi na ujuzi miongoni mwa watumishi wa umma na watanzania kwa
jumla. “Hiki kilikuwa ni kilio chetu cha siku nyingi, sasa kimesikilizwa, ni
matumaini yangu kuwa Makatibu Mahsusi wengi wataichangamkia fursa hii,”alisema.
Katibu Mkuu huyo wa
TAPSEA alitoa wito kwa Makatibu Mahsusi kuichangamkia kozi hiyo kwani itaongeza
uwezo wao wa utendaji wa kazi.
Alisema kozi hiyo ni
fursa nzuri kwa Makatibu hao kwani itawasaidia sana katika kuongeza weledi na
ufanisi kazini.
Baadhi ya Watumishi wa Umma na wananchi
wamekipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma kwa kuanzisha masomo ya Shahada katika
fani hizo na kusema kwamba mafunzo hayo ni hatua kubwa katika mchakato wa
kuendeleza taaluma ya elimu hapa nchini.
Pamoja na kutoa Mafunzo ya muda mrefu
na muda mfupi majukumu mengine ya Chuo cha
Utumishi wa Umma Tanzania ni kutoa Huduma ya Shauri za Kitaaluma, Tafiti na
Machapisho mbalimbali yanayohusiana na uendeshaji wa Utumishi wa Umma.
Mafunzo ya muda mfupi yanatolewa kwa Watumishi wa Umma pamoja na
watumishi wa sekta binafsi ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao ya
kila siku kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Mafunzo yatolewayo na Chuo cha Utumishi
wa Umma Tanzania yamejikita katika maeneo ya Menejimenti, Utawala na Uongozi, Usimamizi
wa Rasilimali Watu, Utunzaji wa
kumbukumbu Taarifa na Nyaraka, Usimamizi wa Fedha, Uendeshaji wa Ofisi,
Ununuzi na Ugavi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
|
No comments:
Post a Comment