Viongozi
wa umoja wa Ulaya wameungana kumuunga mkono waziri mkuu wa Uingereza
Theresa May katika kuilaumu nchi ya Urusi kwa shambulio la sumu kusini
mwa jiji la London na kukubaliana kumuitisha balozi wao wa Moscow kwa
majadiliano zaidi.
Baadhi
ya nchi nazo zimeanza kufikiria kuchukua hatua kama za Uingereza za
kuwafurusha wanadiplomasia wa Urusi, huku nchi za Lithuania na Ufaransa
zikiwa nchi za awali kuonesha kutaka kufanya hivyo.
Waziri
mkuu wa Uingereza Theresa May aliwaambia wenzake wa umoja wa Ulaya kuwa
ni muhimu kuungana kupinga tukio la Machi 4 ambapo jasusi wa zamani wa
Urusi Sergei Skripal na mtoto wake Yulia walipewa sumu iliyowaathiri
mishipa ya fahamu kwenye mji wa Salisbury.
Katika
mkutano wa wakuu wa nchi za umoja wa Ulaya uliofanyika jijini Brussels
hapo jana, viongozi wa nchi 28 wametangaza kuiunga mkono Uingereza na
kukubaliana kuwa kuna uwezekano mkubwa utawala wa Moscow ulihusika na
kwamba hakuna maelezo mengine yanayoweza kupindisha ukweli.
Viongozi
hao wameahidi kuchukua hatua za pamoja na waziri mkuu wa Uholanzi Mark
Rutte amesema wamekubaliana kumuita balozi wao mjini Moscow kwa
majadiliano zaidi.
"Baadhi
ya nchi wanachama wanaangalia uwezekano wa kuwafurusha wanadiplomasia
wa Urusi kwenye nchi zao au kuwatisha wanadipolomasia wao," imesema
taarifa ya umoja wa Ulaya.
Utawala
wa Moscow unakanusha vikali madai kuwa ulihusika kwenye shambulio la
sumu la London ambapo inadaiwa kuwa sumu aina ya Novichok
inayotengenezwa na nchi hiyo ndio iliyotumika.
Waziri
mkuu May amewaambia viongozi wenzake kuwa ni lazima ziungane katika
kuikemea nchi ya Urusi na kuonya kuwa ikiwa watafumbia macho matendo
kama haya, nchi hiyo itaendelea kuwa tishio kwa miaka mingi ijayo.
Jasusi
Skripal na mwane bado wako hospitalini wakipatiwa matibabu baada ya
kupatikana wakiwa wamezimia kwenye bustani moja ya mapumziko licha ya
polisi aliyekuwa ameathiriwa na sumu hiyo wakati akiwahudumia, jana
akiruhusiwa kutoka hospitalini.
No comments:
Post a Comment