Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali
imeeleza kuwa haiwezi kuhamisha jukumu la kulipa pensheni ya Wastaafu
wa Shirika la Posta na Simu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwenda kwenye mojawapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuwa zoezi la
kuunganisha Mifuko ya Pensheni halijakamilika.
Hayo
yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa
Ludewa Mhe. Deo Ngalawa (CCM), aliyetaka kufahamu, lini Serikali
itakuwa tayari kuhamisha jukumu la kuwalipa Wastaafu wa lililokuwa
Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki kwenye moja wapo ya Mifuko
ya Hifadhi ya Jamii.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji
alisema kuwa Serikali kupitia Shirika la Posta inaendelea na jukumu la
kuwalipa pensheni ya kila mwezi Wastaafu wa shirika hilo.
“Uamuzi
wa kuhamisha au kuendelea na utaratibu wa sasa utatolewa baada ya zoezi
la kuunganisha mifuko ya pensheni kukamilika”, alisema Dkt. Kijaji.
Katika
maswali ya nyongeza Mhe. Ngalawa alihoji kwakuwa Shirika la Posta
limekuwa likisuasua katika kujiendesha na miongoni mwa mambo
yanayosababisha ni ulipaji wa pensheni za Wastaafu hao, Serikali haioni
ni wakati wa kulitua mzigo Shirika hilo na kuchukua jukumu hilo.
Mhe.
Ngalawa alieleza kuwa kuanzia mwaka 2015 malipo ya pensheni kwa
Wastaafu yalipanda kutoka Sh. 50,000 hadi Sh. 100,000 lakini kuna baadhi
ya Wastaafu hawajabadilishiwa pensheni zao. Alitaka kujua lini Serikali
itabadilisha pensheni hizo ili ziwe sawa kwa wote.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa baada ya Shirika la Posta kulipa Wastaafu
huwasilisha madai yake Hazina na Serikali imekuwa ikirejesha fedha hizo
kwa wakati na hakuna madai ya ziada.
Alifafanua
kuwa Serikali kupitia Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii imekuwa ikilipa
ongezeko la pensheni kwa Wastaafu kwa wakati, na kukiri kuwa Wastaafu
wachache wamekuwa wakipeleka kesi za kutoongezewa pensheni zao kutokana
na sababu mbalimbali.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa Hazina imekuwa ikipokea malalamiko hayo na
kuyashughulikia, ametoa wito kwa Wastaafu wote yenye malalamiko wafike
Hazina ili waweze kusaidiwa.
No comments:
Post a Comment