RAIS
John Magufuli amewapongeza wananchi wa wilaya za Mbulu, Babati na
Hanang’ mkoani Manyara na Karatu mkoani Arusha zinazounda Jimbo la Mbulu
kwa kumpata askofu wa tano wa Jimbo hilo Anthony Lagwen.
Waziri
wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi ambaye alimwakilisha
Rais Magufuli aliyasema hayo jana mjini Mbulu Mkoani Manyara, kwenye
tukio la kusimikwa kwa askofu Lagwen.
Waziri
kabudi alisema pamoja na kuwapongeza, kanisa katoliki limekuwa msaada
mkubwa kwa serikali kwa kutoa huduma ya elimu, afya na maji hasa kwa
watu wa kawaida.
Alisema
jimbo la Mbulu linaloundwa tangu mwaka 1953 limekuwa mfano wa kuigwa
katika kuhakikisha jamii ya eneo hilo inapata huduma za kiroho na
kimwili.
“Tunapongeza
kanisa katoliki jimbo la Mbulu kwa kutoa huduma za afya ikiwemo
hospitali za misheni za Dareda na Bashnet wilayani Babati,” alisema.
Alipongeza
jimbo hilo kumiliki kituo cha redio Habari Njema ambacho kwa namna moja
au nyingine kinatoa huduma ya uinjilishaji na kuhabarisha jamii.
“Kituo hicho cha redio kiendelee kusisitiza amani kwani bila uwepo wa amani hakutawezekana kufanyika chochote,” alisema.
Alisema
taasisi za dini kwa kiasi kikubwa zimechangia maendeleo mengi na ustawi
wa jamii hivyo serikali itaendelea kushirikiana kwa pamoja ili
kuhakikisha jamii inasonga mbele.
Askofu
mkuu wa Jimbo kuu la Dar es salaam, mwadhama Policarp Kardinali Pengo
alisema japokuwa askofu Lagweni ni mzaliwa wa jimbo la Mbulu lakini
atakumbana na changamoto zile zile wanazokumbana nazo maaskofu ambao
wanaongoza majimbo ambayo hawajazaliwa.
“Mimi
siwezi kuona Sumbawanga ndiyo bora zaidi kuliko sehemu ninayoongoza
waumini hivyo nawe waongoze waamini kama inavyopaswa kuwaongoza,”
alisema Kardinali Pengo.
Rais
wa baraza kuu la maaskofu wakatoliki nchini (TEC) askofu wa jimbo la
Mpanda, Gervas Nyaisonga alisema askofu Lagwen ameteuliwa na Baba
mtakatifu papa Francisco wakati huu ambapo wanasherehekea jubilee ya
miaka 150 ya uinjilishaji.
Askofu
Nyaisonga alisema askofu Lagwen baada ya kupata nafasi hiyo anapaswa
kuwaangalia usoni waumini ili kuzidi kuwajenga kiroho.
Mkuu
wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alisema serikali ya mkoa huo
itashirikiana na jimbo hilo katika kufanikisha ustawi wa wananchi wa
eneo hilo.
Mnyeti
alisema askofu Lagweni amepata daraja hilo la uaskofu ambapo ni heshima
kwa wananchi wa Mbulu, Manyara na Tanzania kwa ujumla.
“Japokuwa
wewe umezaliwa katika jamii ya wairaqw hata ungekuwa mmeru au msukuma
lakini kwa kuwa umeteuliwa kuwa askofu wa Mbulu, umepakwa mafuta kwa
uwezo wa roho mtakatifu,” alisema Mnyeti.
Akizungumza
baada ya kusimikwa askofu Lagwen alisema anamuomba Mungu amsaidie
kutimiza wajibu wake mpya wa kiroho katika kuwahudumia waamini wa eneo
hilo.
Askofu
Lagwen alisema wanashirikiana na serikali katika kufanikisha huduma
mbalimbali na miradi ya elimu, afya, maji, mazingira, habari na
nyingine.
Aliwashukuru
wote walifanikisha tukio hilo na akawaahidi kuwa atatoa ushirikiano
unaostahili kupitia nafasi yake kwa upendo na umoja watumikie.
Askofu
Anthony Lagwen alizaliwa Julai 5 mwaka 1967 kwenye Kijiji cha Tlawi,
wilayani Mbulu mkoani Manyara na kuanza masomo ya elimu ya msingi na
masomo ya sekondari katika seminari ndogo ya Sanu, Jimbo Katoliki la
Mbulu.
No comments:
Post a Comment