WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wanaoshiriki kozi fupi ya tano
ya viongozi wahakikishe watakaporudi kwenye maeneo yao ya utendaji wawe
wamebadilika kimtazamo, kihoja, kiushauri pamoja na utoaji maamuzi.
Ameyasema
hayo leo (Jumatatu, Agosti 13, 2018) wakati akifungua kozi ya tano ya
muda mfupi ya viongozi inayofanyika katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi,
Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu amesema chuo hicho kilianzishwa kwa lengo la kulisaidia Taifa
kujenga uwezo wa viongozi ili wanaohitimu mafunzo hayo wawe na uchambuzi
wa kina na wa kimkakati ili kuweza kutatua mambo mbalimbali ya usalama
wa Taifa na matatizo yanayotakiwa kushughulikiwa kimkakati.
“Chuo
hiki kilianzishwa ili kuwaleta washiriki kutoka taasisi zote za
Serikali na sekta binafsi waweze kujadili mambo mbalimbali ya kimkakati
ili wanapokuwa wanatekeleza wajibu wao watambue kuwa ni kwa kiasi gani
matokeo ya maamuzi yao yataathiri mambo ya kijamii, kiuchumi, uhusiano
wa kidiplomasia na siasa za ndani kwa ujumla wake”.
Amesema
ushirikiano kuhusu kutatua matatizo uanze wakati wa mafunzo hayo na
uendelee hata hapo baadaye watakaporejea kwenye maeneo yao ya kazi.
“Sisi viongozi wenu tunatarajia kuona kuwa mtakapohitimu mafunzo haya
mtakuwa mmebadilika kimtizamo na kwamba taasisi zenu zitakuwa kwenye
nafasi nzuri ya kuzungumza lugha moja”.
Waziri
Mkuu amesema suala hilo ni muhimu sana katika kusukuma maendeleo ya
nchi kwa haraka hususan wakati huu ambao Serikali inalenga kukuza uchumi
wa viwanda, ambapo amewataka viongozi hao watambue kwamba changamoto za
sasa ni mtambuka na hivyo, si rahisi kutatuliwa na taasisi moja moja.
“Changamoto
hizi zimebadili hali ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na uharibifu wa
mazingira, ongezeko la watu, uhaba wa ajira, makosa ya kimtandao,
ugaidi, na mengine mengi ambayo yote zinahitaji mikakati ya pamoja ili
kuweza kukabiliana nayo”.
Awali,
Mkuu wa chuo hicho Luteni Jenerali, Paul amesema mafunzo hayo
yanayoanza leo Agosti 13 yanatarajia kuisha Agosti 17, ambapo mafunzo
hayo yamelenga kuwanoa na kuwawezesha washiriki kujua mambo ya Usalama
wa Taifa na uzalendo kwa nchi.
Pia
watajifunza namna ya kuendesha Serikali kwa kutumia mikakati mbalimbali
pasipo kuathiri usalama pamoja na kupata uzoefu katika mambo mbalimbali
na kuwafanya wawe na uwezo wa kutengeneza, kuendeleza na kusimamia
utekelezaji wa mikakati inayolenga kujenga na kuimarisha Usalama wa
Taifa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 13, 2018.
No comments:
Post a Comment